Quantcast
Channel: Tanzania Sports News, Sports News, Tanzania Sports, Tanzania News, Sports Tanzania.
Viewing all 166 articles
Browse latest View live

Kipigo Yanga:Nyufa ukuta wa Berlin zatia hofu

$
0
0
Mwandishi Wetu
KIPIGO cha mabao 3-0 walichokipata Yanga kutoka kwa Mtibwa Sugar kimewaacha mashabiki wao njia panda kuhusu ubora wa safu ya ulinzi ya timu hiyo iliyoruhusu mabao 9 katika mechi 13 hadi sasa.

Yanga ambayo msimu huu iliwasajili mabeki Kelvin Yondani (Simba), Mbuyu Twite (APR), David Luhende (Kagera Sugar) na Juma Abdul (Mtibwa Sugar) ilionekana kuwa ni moja ya timu yenye ngome imara zaidi baada ya kuruhusu mabao manne tu kwenye mashindano ya Kombe la Kagame.

Safu hiyo ya ulinzi ya Yanga inayoongozwa na nahodha Nadir Haroub,  Yondani, Twite,  Abdul na Luhende Jumatano ilionekana kuwa chochoro mbele ya washambuliaji wa Mtibwa Sugar, Hussein Javu na Dickson Daud.

Kipigo cha mabao 3-0 walichokipata Yanga kiwewashtua mashabiki pamoja na kocha wao Mbelgiji Tom Saintfiet aliyeahidi kulitafutia ufumbuzi suala hilo haraka.

Mashabiki wa Yanga kwa nyakati tofauti waliwalaumu mabeki hao kwa kufanya makosa yaliyowapa nafasi washambuliaji wa Mtibwa Sugar kupata mabao matatu huku mawili yakipachikwa nyavuni na Javu na moja likifungwa na Daud.

Kocha wa Yanga, Saintfiet hata hivyo amewaomba radhi mashabiki wa timu  yake na kuahidi kurekebisha haraka mapungufu ya kikosi chake.

Saintfiet alisema kuwa kitendo cha kupoteza mchezo tena kwa kipigo kikubwa kama hicho kimemuumiza na kumkosesha raha kwa vile mazingira ya mchezo yalikuwa na nafasi kwa kikosi chake kuibuka na ushindi.

"Najua mashabiki wetu wameumizwa sana na matokeo haya na wanayo haki la kulalamika kwakuwa faraja yao ni kuona timu inashinda na siyo vingenevyo, lakini niseme kwamba hata mimi nimeumia na ninachoweza kusema naomba watusaheme,"alisema Saintfiet.

Alisema,"ukweli ni kwamba sisi ndiyo tulikuwa na kila sababu ya kushinda, tulitengeneza nafasi nane hatukuitumia hata moja kufunga, tukapata penati pia tukakosa, wenzetu walitengeneza nafasi nne wakapata mabao matatu hii inaonyesha hatukuwa makini."

Saintfiet alisema,"tunatakiwa kujitazama upya, tukiendelea kuangalia matokeo mazuri ya siku haitatusaidia, yaani umakini haupo kabisa na hii ni kutokana na kila mchezaji kujiona yeye nyota, angalia kama lile goli la pili lilikuwa la kizembe kabisa lakini tulishindwa kulizuia."

Kocha huyo alisema kuwa ikiwa wachezaji wake hawatabadilika na kutambua wajibu wao wanapokuwa uwanjani, itakuwa vigumu kufikia  malengo waliyojiwekea ya kuhakikisha ubingwa unarejea mikononi mwao.

Naye mshambuliaji Hamis Kiiza aliwaomba radhi mashabiki na kuwataka kuwa na subira kwa kuwa ligi ndiyo kwanza imeanza.

Kiiza alisema anaomba radhi kwa kukosa penalti pamoja na kupoteza mchezo huo, lakini siyo sababu ya kukata tamaa bali wawe kitu kimoja wakati huu timu inapohitaji umakini zaidi na ushirikiano baina yao na viongozi wao.

Shabiki Hassan Omari akizungumzia pambano la Yanga na Mtibwa alisema," ule ni uzembe wa mabeki wetu kwani ukiangalia bao la kwanza mfungaji alikuwa peke yake hakubugudhiwa hata kidogo na hata mabao mawili yaliyofungwa na Javu ni makosa yao wenyewe walinzi hauwezi kumlaumu kipa kabisa.”

Naye Jackson Tesha alisema," Yanga walibweteka na kuidharau Mtibwa Sugar na walikuja hapa kuchukua pointi kirahisi."

Tesha alisema pamoja na uzembe wa wachezaji, lakini kocha Tom Saintfiet alifanya makosa kwa kuchezesha wachezaji kwenye nafasi ambazo sio zao za kila siku.

"Kitendo cha Mbuyu Twite kucheza kama beki namba tatu badala ya namba nne na tano kilimfanya Mkongo huyo kushindwa kucheza kwa kiwango chake,"alisema Tesha.

Katika hatua nyingine uongozi wa Yanga unatarajia kukutana leo na benchi la ufundi la timu hiyo kwa ajili ya kujadili matokeo mabovu ya timu yao kabla ya kuivaa JKT Ruvu kesho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Imeandaliwa na Juma Mtanda, Morogoro na Sosthenes Nyoni, Jessca Nangawe.

Hart: Balotelli hakosi penalti

$
0
0

LONDON, England
KIPA wa Manchester City, Joe Hart amesema hategemei hata siku moja kumwona Mario Balotelli akipiga penalti na kukosa kwa sababu ya ya utulivu wake wakati wa kupiga.

Katika mechi dhidi ya Borussia Dortmund Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano wiki hii, Balotelli aliiokoa timu yake na kipigo baada ya kufunga penalti.

Balotelli alipiga penalti hiyo kiufundi akimchambua kipa Weidenfeller na kufunga bao la kusawazisha. Amefunga penalti zote nane alizopiga akiwa na City.

Hart anakumbuka siku aliyodaka penalti ya Balotelli wakiwa kwenye mazoezi.

Balotelli aliwahi kumfunga kipa huyo wakati wa mikwaju ya penalti kati ya Uingereza na Italia wakati wa fainali za Kombe la Mataifa ya Ulaya zilizomalizika katikati ya mwaka huu.

"Mario hakosi penalti. Namtegemea sana. Anatulia na anapiga kiufundi," alisema Hart.

Barca kwa Real, Milan yaivaa Inter

$
0
0

MADRID, Hispania
'HAYAWI hayawi....sasa yamekuwa.' Ndizo kauli zitakazotawala vinywani mwa mamilioni ya mashabiki wa soka watakao kaa kando ya televisheni zao kushuhudia mechi za kuvutia zaidi duniani kati ya Barcelona na Real Madrid na AC Milan dhidi ya Inter Milani hapo kesho.

Macho na masikio ya mashabiki wengi yatakuwa nchini Hispania kwenye mechi ya  'El Clasico' kutokana na ushindani na burudani kutoka kwa Lionel Messi  dhidi ya Ronaldo, kuliko jijini Milan kutokana na soka ya Italia  kuporomoka kwa kiwango kikubwa katika miaka ya karibuni.

Kikosi cha Jose Mourinho kilichofufuka upya baada ya kuanza vibaya ligi, wataingia uwanjani wakifahamu kufungwa kwenye Uwanja wa Nou Camp kutawafanya kuwa nyuma ya Barcelona kwa pointi 11.   

Misimu mitatu iliyopita, yaani kabla ya msimu uliopita, Barcelona ilikuwa ikiwazidi Real kwa pointi nane au zaidi na walifanikiwa kutwaa ubingwa wa La Liga.

Ingawa ni mapema kuindoa Real Madrid katika mbio za ubingwa, lakini timu hiyo imekuwa ikifanya vibaya katika mechi za karibuni. Ilifungwa ikiwa ugenini na Getafe na Sevilla na ilitoka sare katika uwanja wa nyumbani dhidi ya Valencia.

Vinara wa msimamo Barca, imeonyesha kasi kubwa na imeshinda mechi sita za mwanzoni.  
"Tunajitahidi kushinda katika kila mechi," alisema Cesc Fabregas Jumanne wiki hii baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Benfica kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kocha wa Barcelona, Tito Vilanova yupo katika msimu wa kwanza kwenye kikosi hicho na tayari ameonja kipigo cha Real Madrid ambao walitwaa ubingwa wa  Super Cup.  

Vilanova ana wasiwasi kuhusu mabeki baada ya beki wa kati  Carles Puyol kuumia kiwiko na Gerard Pique ameumia mguu.

Pique ana nafasi ndogo ya kurudi uwanjani, lakini Barcelona ina mchezaji mpya  Alex Song upande wa nyuma akiwa na   Javier Mascherano, muungano huo utampa kazi ngumu  Cristiano Ronaldo na wenzake.  

Baada ya kuanza kwa kusuasua, Ronaldo sasa amepata kasi yake ya kuzifumania nyavu, Jumatano wiki hii aliofunga mabao matatu wakati kikosi chake kilipopata ushindi mnono wa magoli 4-1 dhidi ya Ajax Amsterdam kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Matokeo hayo yamemfanya afikishe mabao 12 kwenye michuano yote msimu huu, akiwa juu ya Messi kwa mabao mawili.

Mabao hayo matatu ni ya pili ndani ya siku nne. Alifunga mabao kama hayo wakati walipoiumiza Deportivo Coruna mabao 5-1. Wakati Ronaldo akifanya mambo hayo, Messi hajafunga katika mechi nne.
Real imeshinda 'Clasicos' mara 88, Barcelona mara 87 na wametoka sare mara 46.

Milan: Ni kawaida kwa mashabiki wa Italia kuwa na hamasa kubwa zinapokutana AC Milan na Inter, lakini safari hii Uwanja wa San Siro unaweza kukosa mashabiki kutokana na timu hizo kufanya vibaya msimu huu.
Milan inakwenda kupambana ikiwa kwenye nafasi ya 11 na pointi saba, wakiwa nyuma ya Inter Milan kwa pointi tano.

Milan imezorota baada ya kuwauza nyota wake Zlatan Ibrahimovic naThiago Silva kwa Paris Saint-Germain.
Mpaka kufikia Jumatano wiki hii, ni tiketi 55,000 ndizo zilizouzwa kwa ajili ya mchezo huo, pamoja na zile 23,700 zinazouzwa tangu mwanzo wa msimu.

Watu 28,000 tu ndiyo walijitokeza kuangalia timu yao ikipata ushindi wa kwanza wa mabao 2-0 dhidi ya Calgliari.

Msimu uliopita watu 79,612 walifika uwanjani kuangalia AC Milan ikichapwa bao 1-0 na Inter, wakati mwaka uliopita watu 80,000 waliingia uwanjani kuangalia mechi ambayo Inter Milan ilichapwa mabao 3-0 kwenye mchezo wa Serie A.
"Nadhani vyombo vya habari ndiyo vinatangaza kwamba tuna mashaka," alisema  Massimiliano Allegri ambaye amekalia kuti kavu tangu kuanza kwa msimu.


"Tunaingia kwenye mechi baada ya kupata ushindi, tunafahamu mechi ya upinzani mkubwa haitabiriki, lakini tutajitahidi kufanya vizuri. 

Azam, Lyon 'kusugua' nyasi leo

$
0
0

Mwandishi wetu
AZAM FC, washindi wa pili Ligi Kuu Bara msimu uliopita, leo wanashuka dimbani kukutana uso kwa uso na African Lyon katika mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Azam iliyong'ang'ana nafasi ya pili ikiwa na pointi 10, endapo itavuna pointi tatu kwenye mchezo huo itafikisha pointi 13  kutishia nafasi ya Simba ambayo pia imejikusanyika idadi hiyo ya pointi.

Hata hivyo ili kufanikisha azma hiyo, Azam ambayo imepachika wavuni mabao saba mpaka sasa, italazimika  kuifunga African Lyon na kuibuka na ushindi wa zaidi ya bao moja kuiondoa Simba kileleni.

Nayo African Lyon inayoshikilia nafasi ya tisa ikiwa na pointi sita, haitakuwa na masihara zaidi ya kulifanya pambano hilo kuwa gumu zaidi.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, kocha wa Azam Boris Bunjak na mwenzake wa African Lyon, Pablo Velez kila mmoja alijitapa kikosi chake kuondoka na pointi tatu.

Wakati mtifuano wa Azam na African Lyon ukiendelea Uwanja wa Taifa, katika mji wa Mlandizi, Pwani timu ya maafande wa Ruvu Shooting itaikaribisha Coastal Union katika pambano litakalopigwa kwenye uwanja wa Mabatini.

Vuta nikuvute ya ligi hiyo itaendelea kesho, ambapo Yanga watakuwa ugenini Bukoba kwenye Uwanja wa Kaitaba kuumana na Kagera Sugar.

Yanga yenye pointi nane na ambayo inaangaika kusaka kasi upya baada ya kuianza ligi kwa unyonge, itahitaji ushindi ili kupunguza pengo la pointi dhidi ya mahasimu wao Simba.

Yanga: Tupo tayari kushuka daraja

$
0
0

Jessca Nangawe na Sosthenes Nyoni
UONGOZI wa Yanga umesema utasimama kwenye mstari wa utamaduni wa enzi wa klabu hiyo kutokuvaa jezi yenye rangi nyekundu, na kwa sababu hiyo haiko tayari kutumia jezi za wadhamini wakuu wa Ligi Kuu Bara, Kampuni ya Huduma za Simu ya Vodacom.

Katika kusisitiza msingi wa uamuzi wao, uongozi umesema uko tayari kwa hatua zozote zitakazochukuliwa dhidi yao na hata ikibidi kushushwa daraja lakini siyo kuvaa jezi za Vodacom zenye nembo ya rangi nyekundu.

Tayari Yanga imecheza mechi mbili za ligi bila kuvaa jezi zenye nembo ya Vodacom, huku wadhamini wao wakiwajibu barua yao kwa kusisitiza hawawezi kuondoa nembo hiyo ambayo walikubaliana nayo wakati wa kuingia mkataba wa pamoja.

Katibu mkuu wa Yanga Lawrance Mwalusako, alisema jana pamoja na vitisho kutoka Shirikisho la Soka Tanzanua (TFF) kutaka kuwashusha daraja na kuwatoza faini, hilo haliwasumbui na badala yake watabaki kwenye msimamo wao wa kuheshimu katiba yao inayotambua rangi za kijani, nyeusi na njano.

"Tumeandika barua kwa wadhamini lakini hawajatuelewa na TFF wametishia kutupa adhabu kututoza faini ikiwa ni pamoja na kutushusha daraja.

"Itoshe kusema kwamba, msimamo wa Yanga uko wazi na unaeleweka kwa kila anayefahamu historia ya timu na katiba yake. Hatuwezi kuruhusu rangi nyekundu," alisema Mwalusako.

Mwenyekiti wa Kamati ya ligi Kuu, Wallace Karia alisema kamati yake itasimama kwenye kanunu za kuiadhibu Yanga iwapo itaendelea kukataa kuvaa jezi za mdhamini.

Kauli ya Karia inafuatia msimamo uliotangazwa hivi karibuni na uongozi wa Yanga kuwa kamwe hawatapokea na kuzitumia katika mechi zao jezi zenye nembo nyekundu zinazotolewa na Vodacom.

Karia alisema anashangazwa kuona  klabu hiyo zinaendelea kukaidi kuvaa jezi zenye nembo ya mdhamini wakati suala linasimama kwenye kanuni.

"Kimsingi suala la Yanga na African Lyon kukataa kuvaa jezi zenye nembo ya mdhamini halijafika kwenye kamati yangu, bado linashughulikiwa na Sekretarieti ya TFF. Likifika kwangu, tutachukua hatua kwa kuzingatia kanuni," alisema Karia.

" Pale hakuna utata, jambo lenyewe ni la kikanuni. Yanga na African Lyon zivae jezi zenye nembo ya mdhamini wa ligi ambayo wao wanashiriki na siyo kinyume chake," alisisitiza Karia.

"Miaka ya nyuma ilikuwa kama hutaki basi hupokei vifaa na kama ukishinda taji hupokei zawadi, lakini kanuni zimebadilika ni lazima klabu zizingatia masharti,".

Karia aliongeza kuwa hata msimu uliopita kamati yake ilishikilia msimamo wa kuzingatia kanuni  baada kuwapo mgogoro wa huohuo kati ya Yanga na Vodacom ingawa baadaye ulimalizika  baada ya pande husika kukubaliana.

"Mwaka jana msimamo wetu ulizitaka klabu kuzingatia kanuni ingawa baadaye Vodacom na Yanga walikubaliana na sisi hatukuwa na kipingamizi.

"Hata safari hii tuliwaambia Yanga wakitaka wakakubaliane na Vodacom kama walivyofanya wakati ule laini siyo vinginevyo," alisema Karia.

Naye Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema kuwa ikiwa klabu hizo zitaendelea na msimamo wao wa kutovaa jezi zenye nembo ya mdhamini, zitaadhibiwa kwa kufuata kanuni ya 38 inayozungumzia hatua za kuchukua kwa  timu iliyokiuka masharti.

"Kanuni ya 38 inaeleza wazi, ukikiuka masharti adhabu ni kulipa faini ya Sh1.5 Milioni kwa kila mchezo na kama itaendelea inaweza kuondolewa kwenye mashindano na au kufungiwa.

Wizara Elimu, Ikulu watamba Shimiwi

$
0
0
Juma Mtanda, Morogoro
TIMU ya soka ya Wizara ya Elimu na  Mfunzo ya Ufundi  wameibuka mabingwa  wa michuano ya Shimiwi 2012 baada ya kuchakaza  Ukaguzi kwa mabao 4-0 kwenye fainali iliyofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Michuano ya Shirikisho la Michezo ya Idara za Serikali, Wizara na Ofisi za Wakuu wa Mikoa(Shimiwi) yamefikia tamati jana kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.

Elimu walianza mchezo huo kwa kasi na kufanikiwa kupata mabao yake kupitia nyota wake Nicholaus Makata, Mussa Lusela na Richard Mwakalinga akishindilia msumali wa mwisho kwa Ukaguzi0.

Nayo Ikulu Sport Club ilifanikiwa kutwaa ubingwa wa michezo miwili ya netiboli na kuvuta kamba wanaume na wanawake.

Ikulu netiboli iliibuka kidedea kwa kutwaa ubingwa huo baada kuifunga Afya Sport Club katika mchezo mkali kwa vikapu 50-32.

Ushindi huo wa Ikulu ulichangiwa na wafungaji wao mahili Monica Kassy na Mwadawa Twalib baada ya kuiongoza vema timu yao kwa kufunga vikapu 14-7 katika kipindi cha kwanza wakati kipindi cha pili wakifunga 30-4, 39-19 na kumaliza kwa vikapu 50-32.

Mabingwa watetezi wa mchezo wa kuvuta kamba Ikulu wanaume waliweza kuibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Hazina Sport Club wakati kwa upande wa mabingwa watetezi katika mchezo huo wa kuvuta kamba wanawake wakishinda kwa idadi kama hiyo dhidi ya Ras Iringa katika michezo ya fainali ya mchezo huo.

Mashindano hayo yalifungwa rasmi jana (juzi) na Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Peter  Ilomo kwa kutoa zawadi ya vikombe kwa washindi wa kwanza hadi tatu katika michezo mbalimbali ukiwemo soka, netiboli, riadha, basikeli, michezo ya jadi, kuvuta kamba na mingine.

Ronaldinho apiga tatu Mineiro ikishinda 6-0

$
0
0
RIO DE JANEIRO, Brazil
RONALDINHO alifunga mabao matatu na kuisaidia Atletico Mineiro kuichakaza Figueirense 6-0 na kusogea kileleni mwa ligi ya Brazil.

Fluminense inaongoza ligi kwa tofauti ya pointi sita kwa Mineiro baada ya mshambuliaji Fred kufunga bao pekee kwenye mchezo wa watani wa jadi wa jiji la Rio dhidi ya Botago 1-0.

Mwanasoka bora wa zamani  wa dunia Ronaldinho alifunga bao la kwanza kwa Mineiro, kwa krosi yake iliyokwenda moja kwa moja wavuni.

Ronaldinho, aliyejiunga na Mineiro akitokea Flamengo mwaka huu, alifunga bao la pili kwa mpira wa adhabu na kuhitimisha bao lake la tatu kwa mkwaju wa penalti. Pia alitegeneza mabao mengine mawili yaliyofungwa na beki Rever na mshambuliaji Bernard kabla ya Carlos Cesar kuhitimisha karamu hiyo kwa kufunga bao la sita.

Mshambuliaji Fred alifunga bao lake katika dakika ya 72, akimalizia pasi krosi ya winga Wellington Nem kwenye Uwanja wa Engenhao jijini Rio.

Makipa wa timu zote mbili walifanya kazi kubwa huku kip wa Flu, Diego Cavalieri akipangua mashuti akiwa yeye na viungo Fellype Gabriel na Elkeson baada ya kutegenezewa pasi nzuri na mkongwe Clarence Seedorf.

Kipa wa Botafogo, Jefferson aliokoa kwa ustadi mkubwa kichwa kilichopigwa na beki Digao akiunganisha krosi ya Deco.

Mshambuliaji wa Brazil, Luis Fabiano alifunga mabao mawili kuiongoza Sao Paulo kuichapa Palmeiras 3-0. Huku kiungo wa zamani wa Arsenal, Denilson akifunga bao moja kwa Sao Paulo.

Palmeiras walipata pigo baada ya beki wao Jose Manuel Barbosa kutolewa nje kwa kadi nyekundu katika dakika ya 53, ikiwa ni kadi ya njano ya pili.

Rick Ross awaachia ujumbe mzito vijana

$
0
0
Herieth Makwetta
DAKIKA 45 alizozitumia mwanamuziki kutoka nchini Marekani, William Leonard Roberts, Rick Ross akiwa jukwaani aliweza kuburudisha na kuelimisha maelfu ya vijana waliojitokeza katika Tamasha la Serengeti Fiesta lililofanyika usiku wa kuamkia jana katika Viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam.

Rapa huyo anayeshika nafasi za juu kati ya wanamuziki wa kimataifa hivi sasa, alisikika mara kwa mara akiwataka vijana kujituma katika kufanya kazi kwa bidii ili kuyafikia mafanikio kwa njia za halali.

"Unatakiwa kufanya kazi mwanamume, fanya kazi jitume na teseka katika kutafuta maisha, mimi ni boss, lakini nilikuwa boss kabla sijapata maisha, nilijituma katika kutafuta," ni maneno aliyoyarudia mara kwa mara Rick Ross kila alipomaliza kuimba nyimbo.

"Ninahisi upendo wa hali ya juu, hii ni mara yangu ya kwanza kufika katika nchi hii ya watu wakarimu, najua nchi itazidi kupata maendeleo na baadaye mtafikia malengo ikiwa vijana mtajituma," alisema mwanamuziki huyo mwenye miaka 36, ambaye aliimba vibao kama The Boss ft T.Pain, Hustlin, Aston Martin Music, I m ma Boss, Blow Money Fast (BMF) na nyinginezo nyingi.

Rick Ross ambaye alipanda jukwaani saa nane na dakika 20 usiku alifurahiwa zaidi na mashabiki ambao awali walimwona Rick Ross bandia (Mtanzania anayefanana na Rick Ross) aliyepanda saa saba kamili usiku huo.

Rick Ross aliimba vibao vyake vilivyopo kwenye chati pekee na kushuka jukwaani saa tisa na dakika tano usiku huku mashabiki wakiwa bado wana kiu ya kuendelea kusikiliza baadhi ya vibao vyake vilivyosalia.

Msanii Mwasiti Almasi alipata wakati mgumu baada ya kupokea kijiti kutoka kwa Rick Ross hali iliyomfanya aimbe kwa kutetemeka jukwaani huku baadhi ya mashabiki wakijikusanya na kutoka uwanjani.

Kupungua kwa mashabiki kulileta ahueni kwa baadhi ya mashabiki  kwa sababu awali Leaders ilikuwa imejaa watu wengi, huku wasanii wengine waliokuwa wamesalia wakiendelea kutoa burudani.

Katika tamasha hilo usalama ulizingatiwa sana na kulikuwa na askari zaidi ya 250 ambao walikuwa wamezagaa hivyo kuhakikisha usalama wa kutosha kwa raia.

Mazingira ya uwanja yalikuwa salama ingawa kulikuwa na hatari kutokana na uwanja kujaa kupita kiasi na watu walikuwa wakisukumana ovyo mara baada ya Rick Ross kupanda jukwaani.

Burudani hiyo ilifunguliwa na Kundi la Makomandoo kabla ya kumpisha Rich Mavoko, Recho, Linah, TID, Nay Wa Mitego, Mwana FA, Stamina Wanaume Family, AT, Shilole, Nikki wa Pili na Joh Makini kabla ya kupanda jukwaa Rick Ross.

Baada ya mwanamuziki Rick Ross kuimba alimwachia kijiti Mwasiti, Dayna, Fid Q, Quick Rokar, Country Boy, Darasa, Sheta, Mabeste, Juma Nature, Nuru, Ommy Dimpoz, Diamond na wengineo.

Yanga yashindwa kukodi ndege

$
0
0
Mwandishi Wetu
WAKATI uongozi wa Yanga ukijinasibu kuwasafirisha wachezaji wake kwa ndege ya kukodi, imebainika kuwa huo ni uongo kwani wachezaji hao na viongozi wawili wa timu hiyo walipanda ndege ya abiria wa kawaida.

Yanga waliondoka juzi Jumamosi na ndege ya Shirika la Precision kwenda Mwanza kabla ya kuunganisha na charter kwenda Kagera na kufikia kwenye Hoteli ya Smart.

Wachezaji wa Yanga wakiwa na kocha msaidizi wa timu hiyo waliangua kicheko pale walipoulizwa kulikoni kujazana
kwenye ndege ya abiria wa kawaida badala ya ndege yao ya kukodi.

Wachezaji walisema viongozi wao wamekuwa watu wa maneno mengi huku wakifanya mambo tofauti.

Mmoja wa wachezaji wa Yanga alisema, "Ndiyo wamewadanganyeni wanatukodia ndege? Achaneni nao hao wana maneno mengi utekelezaji sifuri."

Mwingine alisema,"Yaani hawa viongozi wangekuwa wanatekeleza yote wanayosema tungekuwa mbali sana, lakini ahadi nyingi utekelezaji hakuna tumeshawazoea uongo wao.”

Mwingine alisema, "Haaa sisi tunawaita wazee wa 'sound', wakakodi ndege wao? Hembu usinichekeshe huyo kiongozi aliyesema anakodi ndege ni nani jamani, dah viongozi wetu kwa maneno! Duh hiyo kali, kwa hiyo wakasemaje wanatukodia
ndege?" Alisema huku akiangua kicheko.

Kocha msaidizi wa timu hiyo Felix Minziro aliposikia kauli hiyo ya kukodi ndege aliangua kicheko huku akishikilia mbavu
zake akiwa amesimama na Kocha mkuu wa Yanga, Enerst Brandts  ambaye hakuelewa kilichokuwa kikiendelea zaidi ya kutabasamu muda wote.

Yanga iliwasili Jumamosi saa tatu asubuhi kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza na kuunganisha kwa ndege ndogo kuelekea Kagera ikiwa na kikosi cha wachezaji 18 huku wachezaji waliosalia wakitarajiwa kuwasili leo na basi walilopewa na mdhamini wao Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro.

Kikosi cha Yanga kilichowasili juzi kwa ndege ni Kipa Yaw Berko, Ally Mustapha,  Haruna Niyonzima, Omega Seme, Athuman Idd 'Chuji', Shamte Ally, Stephano Mwasika, Nurdin Bakari, Haruna Niyonzima, Nadir Haroub 'Canavaro'' na Jerry Tegete.

Pia wapo wachezaji wao wapya ambao ni Mbuyu Twite, Didier Kavumbagu, Ladslaus Mbogo, Said Bahanuzi, Juma Abdul, Frank Dumayo, David Luhende na Nizar Khalfan.
 
Huku viongozi waliosafiri na timu ukiachia benchi la ufundi ni wajumbe wa kamati ya utendaji, Tito Osoro na Musa Katabalo.

Samata awania tuzo mwanasoka bora wa Afrika

$
0
0
Sosthenes Nyoni
SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limemteua mshambuliaji wa  TP Mazembe na Tanzania, Mbwana Samata kuwa miongoni mwa nyota 32 watakaowania tuzo ya mwanasoka bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani ya Afrika.

Hii ni mara ya kwanza kwa mchezaji wa Tanzania kuingia kwenye orodha hiyo ya wachezaji wanaowania tuzo ya Afrika kwa wachezaji wa ndani.

Katika taarifa iliyotolewa mwishoni mwa wiki na CAF, ilivitaja vigezo vilivyotumika kumjumuisha Samata kwenye orodha yake kuwa ni mchezaji kijana aliyeibuka na kuwa nyota katika kikosi cha TP Mazembe tangu alipojiunga nayo mwaka 2011.

Pia, lilimtaja Samata kama miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha TP Mazembe akiwa ameifungia mabao sita katika mechi mbalimbali za michuano ya kimataifa.
Hivi karibuni Samata aliingia kwenye  orodha ya wafungaji bora 71, duniani sambamba na Lionel Messi, Neymar na Cristiano Ronaldo.

Mbali ya Samata, TP Mazembe imefanikiwa kuingiza jumla ya wanandinga watano kwenye kinyang'anyiro hicho cha kumsaka mwanasoka bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani.

Wengine ni mshambuliaji raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Tresor Mputu, beki Stoppila Sunzu, kiungo Rainford Kalaba na mshambuliaji Given Singuluma wote raia wa Zambia.

Orodha kamili ya nyota 32 wanaowania tuzo hiyo na klabu zao na nchi wanazotoka ni Mbwana Samata (TP Mazembe, Tanzania),  Abdelmoumen Djabou (Club Africain, Algeria), Ahmed El-basha(Al-Merreikh, Sudan), Ahmed Zuway (CA Bibertin, Lybia), Abdoulrazak Fiston (Lydia Adacademic, Burundi), Alou Bagayok (Djoliba, Mali), Moxolisi Mthethwa (Royal Leopard, Swaziland) na Oboaboa Godfrey (Sunshine Stars, Nigeria).

Pia yupo Alula Girma (St George, Ethiopia), Azuka Boko Izu (Sunshine Stars, Nigeria), Boubacar Bangolula (Djoliba, Mali), Edward Sadomba (Al Hilal, Zimbambwe), Essam El Hadary (El Merreikh, Misri), Emmanuel Clottey (Esperance, Ghana), Given Singuluma (TP Mazembe, Zambia), Omar Mohamed Bakheet(Al Hilal, Sudan), Rainford Kalaba (TP Mazembe, Zambia) na Razak Yakubu (Al Ahly Shandy, Ghana).

Wengine ni Amouda Ahmed Elbashir (Al Ahly Shandy,Sudan), Arrison Affur (Esperance,Ghana), Ismailia Diara (Cercle Olympique de Bamako,Mali), Joao Hernani (Interclub,Angola), Mohamed Aboutreika (Al-Ahly,Misri), Mongezi Bobe (Black Leopards,Afrika Kusini), Mudather El-Taieb (Al Hilal, Sudan) na Solomon Asante (Berekum Chelsea, Ghana).

Orodha hiyo inakamilishwa na Stopila Sunzu (TP Mazembe, Zambia), Taboko Eric Nyemba (AC Leopard Dolisite, DRC Congo), Tresor Mtupu (TP Mazembe, DRC Congo), Walid  Hicheri (Esperance, Tunisia),  Yannick N'Djeng (Esperance,Cameroon) na Youssef Msakni (Esperance, Tunisia).

Simba yaua, Mgambo, Toto zaona mwezi

$
0
0
*Yanga yaivaa Kagera Sugar leo
Waandishi Wetu
MABINGWA watetezi Simba waliwasambaratisha wachezaji tisa wa JKT Oljoro kwa mabao 4-1, huku Mgambo Shooting na Toto African zikipata ushindi wa kwanza kwa kuzichapa Polisi Moro na JKT Ruvu katika mechi za Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Kiungo Amri Kiemba wa Simba ameendelea kung'ara baada ya kufunga mabao mawili wakati Emmanuel Okwi na Felix Sunzu kila mmoja akifunga bao moja huku Paul Nonga akifunga bao pekee kwa Oljoro katika mchezo ambao mwamuzi Amon Paul alitoa kadi mbili nyekundu na tano za njano.

Wachezaji wa Oljoro waliopewa kadi nyekundu ni kipa Shaibu Issa na beki Meshack Nyambele huku Kalage Gunda na Nyambele wa Oljoro pamoja na Okwi wa Simba wakipewa kadi za njano.

Kwa matokeo hayo Simba imeendelea kuongoza Ligi Kuu ikiwa na  pointi 16 na kuwaacha watani zao Yanga kwa pointi nane kabla ya mchezo wa leo dhidi ya Kagera Sugar.

Mashabiki wa Simba walisubiri hadi dakika ya 16 kuanza kushangilia bao baada ya kiungo Kiemba kufunga bao la kwanza kwa shuti baada ya kupokea pasi nzuri ya chipukizi Christopher Edward kutoka upande wa kulia.

Dakika chache baadaye, Sunzu aliukwamisha mpira nyavuni dakika 21 akiuunganisha kwa ustaadi krosi Mwinyi Kazimoto, lakini mwamuzi Paul alilikataa bao hilo kwa madai mfungaji alikuwa ameotea.

Ilipofika dakika ya 29 Paul Nonga aliifungia Oljoro bao la kusawazisha, akitumia vizuri mpira uliomponyoka mguuni Shomari Kapombe kisha kumlamba chenga Kaseja na kuutumbukiza mpira wavuni.

Lakini wachezaji wa Simba hawakukata tamaa kwani kiungo Kiemba alifunga bao la pili kwa Simba akiunganisha kwa kichwa mpira uliokolewa vibaya na mabeki wa Oljoro na kuwafanya mabingwa hao watetezi kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-1.

Kipindi cha pili kocha wa Simba, Cirkovic Milovan aliwapumzisha Edward na Paul Ngalema na kuwaingiza Haruna Moshi na Kigi Makasi, huku kocha Mbwana Makata akimtoa Nato Zuberi na nafasi yake kuchukuliwa na Jackson Semfukwe.

Mwamuzi Paul alimuonyesha kadi nyekundu Nyambele ikiwa ni kadi ya njano ya pili baada ya kumchezea vibaya Jonas Mkude dakika 78.

Kutoka kwa mchezaji huyo kulitoa mwanya kwa Simba kwani dakika ya 82 Okwi alifunga bao la tatu akitumia vizuri uzembe wa mabeki wa Oljoro.

PiaSunzu aliipatia Simba bao la nne kwa mkwaju wa penalti baada ya Okwi kuangushwa kwenye eneo la hatari na kipa Shaibu, ambaye pia alitolewa kwa kadi nyekundu.

Tanga: Mgambo Shooting ilipata ushindi wake wa kwanza baada ya kuichapa Polisi Moro kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani,  Tanga.

Mgambo walipata bao lao katika dakika 21, lililofungwa na Salum Kipanga akiunganisha kwa kichwa kona iliyopigwa na Chande Magoja.

Katika mchezo mwingine Toto African iliutumia vizuri uwanja wake wa nyumbani wa CCM Kirumba kwa kuichapa JKT Ruvu kwa mabao 2-1.

Toto walipata bao la kwanza dakika 12 kupitia Severin Constantin na Selemani Kibuta alifunga la pili dakika ya 56, huku lile la Ruvu likifungwa na Amos Mgisa dakika ya 20.

Kutokana na ushindi huo mashabiki wa Toto walichanga sh 95,000 na kuwapa wachezaji kama zawadi yao.

Nayo Prisons walilazimishwa kugawana pointi na Mtibwa Sugar baada ya kutoka suluhu 0-0 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

HAPATOSHI KAITABA
Mabingwa mara 22 Yanga wenyewe watashuka kwenye Uwanja wa Kaitaba leo wakiwa na kumbukumbu mbaya kwenye uwanja huo wakati wakapowakabiri wenyeji Kagera Sugar.

Msimu uliopita Yanga ilipoteza mechi mbili za kanda ya ziwa baada ya kufungwa na Kagera 1-0 na baadaye Toto African 3-2 matokeo yaliyochangia kupoteza ubingwa wao.

Kocha mpya wa Yanga, Ernest Brandts amelalamikia ubovu wa uwanja wa Kaitaba kwa madai kuwa utawazuia wachezaji wake kucheza kwa umakini.

"Uwanja ni mbaya itakuwa vigumu wachezaji wangu kucheza vizuri hapa, lakini tutajitahidi kuhakikisha tunashinda,"alisema Brandts.

Kuhusu suala la kusogezwa mbele kwa mchezo huo kocha Brandts alisema,"nimeelewesha kuwa kuna shughuli za kiserikali, nimeambiwa kwamba kuna Kardinali wa kwanza Mwafrika anazikwa, nimeelewa na hakuna tatizo katika hilo."

Imeandaliwa na Sosthenes Nyoni (Dar), Burhan Yakubu (Tanga), Annastazia Fredy (Mwanza),Godfrey Kahango (Mbeya) na Vicky Kimaro (Bukoba).

Mabondia 13 waitwa timu ya taifa

$
0
0
Imani Makongoro
SHIRIKISHO la ngumi za ridhaa Tanzania (BFT) limewaita mabondia 13 kuunda timu ya taifa ya ngumi za ridhaa kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mashindano ya ngumi Afrika yatakayofanyika mwishoni mwa mwezi huu jijini Cassablanca, Morocco.

Mabondia hao wameteuliwa baada ya kuonyesha uwezo kwenye mashindano ya ubingwa wa taifa yaliyomalizika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Katika kikosi hicho, sura tatu ni ngeni huku mabondia waliowahi kuichezea timu hiyo wakati ikinolewa na kocha kutoka Cuba, Pimentel Hurtado wakirejea tena kwenye kikosi hicho.

Mabondia walioteuliwa na uzani wanaopigania kwenye mabano ni Said Hofu na Hafidh Bamtula (fly kg 49), Sunday Elias na Boniface Mlingwa (ligt fly kg 52), Emilian Patrick na Undule Langson, (bantam kg 56).

Wengine ni Iddi Pialali, Hamis Kitenge na Nasser Mafuru (kg 60), Victor Njaiti na Hashim Saimon (welter kg 64), Seleman Kidunda na Mohamed Chibumbuli (light welter kg 69) na Joseph Martin anayepigania uzani wa kati kg 75.

Mabondia wengine walioitwa kwenye kikosi hicho ni Amos Godwin na Leonard Machichi (light heavy kg 81), Haruna Swanga na nuru Ibrahimu (kg 90) na Maximilian Patrick anayepigania uzani wa 91+.

Katibu mkuu wa BFT, Makore Mashaga alisema uteuzi wa mabondia hao umezingatia vigezo na kusisitiza kwamba umefanywa kwa ushirikiano wa kamati ya ufundi ya BFT na jopo la makocha wa mchezo huo nchini.

"Mchakato wa kuteua timu hiyo umefanyika kwa umakini ili kuhakikisha tunapata timu bora itakayotuwakilisha kwenye mashindano mbalimbali ya kimataifa," alisema Mashaga.

Alisema mabondia hao wataanza kambi mapema kujiandaa na mashindano ya kanda ya sita Afrika, Jumuiya ya madola, Afrika, Olimpiki, Dunia na mashindano mengine ya kimataifa.

Katika hatua nyingine BFT imeteua timu ya ngumi ya taifa ya vijana itakayopeperusha bendera ya taifa kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya vijana ya Zambia utakaofanyika Oktoba 20 jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Mashaga, mbunge wa Kinondoni, Iddi Azan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye mashindano hayo ya kujipima nguvu kwa timu hiyo ya ngumi ya taifa ya vijana.

Chelsea yazidi kunogewa na Falcao

$
0
0

MADRID, Hispania
KLABU ya Atletico Madrid inayokabiliwa na madeni mengi, imesisitiza kuwa mshambuliaji wake Radamel Falcao hataondoka Januari mwakani, lakini kuna habari kwamba Chelsea ina nafasi kubwa ya kumsajili kipindi kijacho cha usajili majira ya joto.

Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Colombia, amekuwa gumzo kubwa tangu akiwa Porto na kiwango chake cha sasa kufunga mabao kama ilivyo kwa Cristiano Ronaldo na Lionel Ligi Kuu Hispania kimempa sifa zaidi na kuzivutia timu nyingi.

Jumanne wiki hii, meneja wa Atletico, Gil Marin alitaja dau kubwa la kuanzia kwa klabu zitakazomtaka, akisema dau hilo kwa kiasi fulani litasaidia kupunguza madeni yanayowakabili.

Klabu hiyo ya Madrid imeelezwa kuwa na madeni ikiwa ni pamoja na kodi. Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) limezuia zawadi za timu hiyo kwa kile ilichoeleza kushindwa kufanya malipo kwa baadhi ya mambo.

Ingawa imetangaza kuendelea kubaki na Falcao msimu huu, lakini ukweli ni kwamba kasi ya madeni inaweza kuwalazimisha kumpiga bei mapema kabla hata ya muda.

Dhamira kubwa ya Falcao ni kucheza Chelsea au Real Madrid kama ambavyo baba yake mzazi pia amekuwa akitaka.
Lakini matajiri wa London, ndiyo wenye nafasi kubwa ya kumalizana na Falcao ingawa pia Manchester City na Paris Saint-Germain nazo zimefungua macho kwa mchezaji huyo na ziko tayari kutoa dau lolote.

"Falcao atabaki hapa, angalau naweza kusema mpaka mwishoni mwa msimu. Lakini kama Atletico haitapata fursa ya kucheza Ligi ya Mabingwa na klabu ikashindwa kumlipa Falcao, bado sidhani kama Real Madrid wanaweza kulipa gharama hizo," alisema Marin.

Wiki iliyopita Falcao alisema: "England? Ndiyo, ipo siku naweza kwenda. Ni sehemu kwenye soka nalolipenda, ipo siku nataka kujaribu.

"Nilipokuwa mtoto nilikuwa naangalia kupitia televisheni. Wachezaji kama Roy Keane, Eric Cantona [Gianfranco] Zola,[Faustino] Asprilla, walinivutia sana na kujifunza mengi. Nadhani nikiwa England, naweza kufunga mabao mengi.

Mataifa zaidi yaalikwa Rock City Marathon

$
0
0
Clara Alphonce
WAANDAAJI wa mbio za marathon za Capital Plus International (CPI), wamewataka wakimbiaji kutoka mataifa mbalimbali kujitokeza katika mashindano yake yanayotarajia kufanyika kwenye jiji la Mwanza Oktoba 28.

Mratibu wa mbio hizo kutoka katika kampuni ya CPI, Grace Sanga aliiambia Mwananchi jana kuwa maandalizi yanakwenda vizuri na kwamba ushiriki wa wanariadha wa kimataifa, utasaidia kuinua mbio hizo.

"Nafikiri ni wakati mwafaka, mbio za Rock City Marathon ambazo kauli mbiu yake “tukuze utalii kupitia michezo” zitakuwa chachu na hamasa kwa wanariadha wetu kufanya vizuri," alisema Sanga.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa hundi ya Sh10mil na fulana 100 katika hafla fupi ya kukabidhi fedha hizo juzi, alisema pia kuwa kuna haja ya wakimbiaji wa Tanzania kujitokeza zaidi kwani ni nafasi yao kuonyesha wanaweza.

Naye Kaimu Meneja Kiongozi Uhusiano na Huduma kwa Wateja, wa Shirika la Hifadhi ya Jamii, NSSF, Theopista Mheta alisema kuwa shirika lake linatambua umuhimu wa michezo mbalimbali nchini ukiwemo wa riadha katika kukuza utalii wa ndani.

 “Tunatambua michezo inachangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza utalii wetu wa ndani hususan riadha lakini pia tuna imani kuwa kupitia mbio za Rock City mwaka huu vipaji vipya vitagundulika.

“Tunaahidi kuendelea kusaidia michezo mingine kwa kuwa pia tunaamini kupitia michezo mbalimbali tunaweza kutangaza vivutio vyetu vya utalii duniani...mbio za mwaka huu zitakazowakutanisha wanariadha mbalimbali kutoka Afrika, Ulaya na Amerika."

Mbali na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) wadhamini wengine ni pamoja na Airtel Tanzania, Parastal Pension Fund (PPF), Geita Gold Mine, African Barrick Gold, Air Tanzania Company Ltd (ATCL), Mamlaka ya Taifa ya Mbuga za Wanyama nchini (TANAPA), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Nyanza Bottles, New Africa Hotel na New Mwanza Hotel.

Waislamu wasusa jezi Newcastle

$
0
0

LONDON, England
BARAZA la Waislamu England (MCB), limewataka wachezaji waumini wa Dini ya Kiislamu wa timu ya Newcastle United inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo, kutovaa fulana za wadhamini wapya wa klabu hiyo, Kampuni ya Wonga, na kinyume na agizo hilo watakuwa wamekiuka sheria za dini hiyo.

Kampuni ya Wonga inayojihusisha na mikopo, imeingia mkataba wa miaka minne na klabu hiyo na kuwekeza kiasi cha paundi 24 milioni kwa ajili ya fulana hizo.

Uamuzi wa MCB unakwenda sambamba na kusambaza ujumbe kwa waumini wengine kususia kuvaa fulana hizo kwa vile kampuni hiyo imekuwa ikitoza riba kwa mkopo wa siku 30.

MCB inapinga mpango wa Wonga kuwakopesha mashabiki wa Newcastle fulana moja kwa paundi 49.99 na kisha kurejesha paundi 71.92 ndani ya siku 30.

Kwa mujibu wa sheria za kiislamu, mtu hapaswi kupata faida kwa kumkopesha mtu kitu. Hii ina maana kwamba mkopo haupaswi kurejeshwa na riba.

Wachezaji waumini wa dini ya kiislamu kwenye klabu hiyo ni pamoja na Demba Ba, Papiss Cisse, Cheick Tiote na Hatem Ben Arfa.


Pesa za Twite bado moto

$
0
0

Clara Alphonce
HUKU Klabu ya Simba ikiendelea kuishinikiza Yanga kuwalipa pesa za usajili wa mchezaji Mbuyu Twite, Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), inajiandaa 'kuihukumu' klabu hiyo ya Jangwani kwa kushindwa kutekeleza agizo walilowapa.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Alex Mgongolwa amesema wanatarajia kukutana wakati wowote kuanzia sasa kujadili hatua za kuchukuliwa dhidi ya Yanga.

Septemba 10 mwaka huu, kamati hiyo ilimuidhinisha Twite kuichezea Yanga, lakini ikiitaka klabu hiyo ya Jangwani kurejesha Simba pesa kiasi cha dola 32,000 alizochukua mchezaji huyo alipoingia mkataba na Simba.

Kamati hiyo pia iliitaka Yanga kumaliza pesa za usajili wa mchezaji David Luhende kutoka Kagera Sugar ndani ya siku hizo 21, lakini mpaka sasa hawajafanya hivyo.

Mgongolwa alisema kamati yake imemwandikia barua Katibu wa TFF, Angetile Osiah kumtaka aitishe kikao ili kujadili suala hilo.

Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema wameshangazwa hatua ya Yanga kukaidi kulipa pesa hizo kama walivyoelekezwa na kamati.

"Tuliiandikia barua TFF Septemba 29 mwaka huu kuwaomba waikate Yanga fedha kwenye mechi yetu na wao ili kufidia deni hilo, lakini TFF hawakufanya hivyo," alisema Kamwaga.

Kaimu Katibu wa Yanga, Lawrance Mwalusako alikerwa na swali aliloulizwa kuhusu lini klabu hiyo itakuwa tayari kulipa madeni fedha hizo.

"Hili ni suala la kiungozi zaidi, siyo jukumu lenu kufahamu, nachofahamu watakamalizana wenyewe," alisema Mwalusako.

Wakati huohuo, wadhamini wa Ligi Kuu Bara, Kampuni ya Huduma za simu Vodacom, imesema iko tayari kukutana na Yanga kujadili suala utata wa jezi.

Yanga imesusa kuvaa jezi za kampuni hiyo zenye nembo ya rangi nyekundu, wakidai kufanya hivyo ni kwenda kinyume na katiba ya klabu ambayo haitambui rangi hiyo.

Kauli hiyo ya Vodacom imekuja siku moja baada ya Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga kutaka pande hizo mbili kukaa chini na kufikia muafaka.

Meneja Masoko wa Vodacom, Kelvin Twisa alisema milango iko wazi kwa Yanga kuja kujadili hoja za udhamini kama wanaona kuna kasoro kati yao.

Kocha Yanga ataka wabadilike

$
0
0
Vicky Kimaro - Mwanza
KOCHA wa Yanga, Enerst Brandts amewataka wachezaji wake Nurdin Bakari na Juma Seif kubadilika huku akifunga milango kwa beki Shadrack Nsajigwa.

Brandts alisema haridhishwi na kiwango cha Nurdin na Seif Kijiko kwa sasa na kuweka bayana kwamba Nsajigwa hana nafasi kwenye kikosi chake.

ìWanatakiwa kubadili uchezaji wao ili wapate nafasi  kwenye kikosi cha kwanza,îalisema kocha huyo.

Kuhusu hatma ya beki Nsajigwa ëFusoí aliachwa kwenye safari ya Kanda ya Ziwa, Brandts alisema sijaona kiwango chake, sijaona umuhimu wa  yeye kuja huku, hapa nipo na wachezaji 20.

Tangu kuanza msimu huu Nsajigwa ameshindwa kupata namba ya kudumu kwenye kikosi cha Yanga baada ya kuwajiliwa kwa Mbuyu Twite na Juma Abdul.

Hivi karibuni Nsajigwa alikaririwa na vyombo vya habari akisema Yanga imesajili vijana wengi wazuri ndio maana amekosa namba kwenye kikosi hicho.

ìNimewapisha vijana waweze kucheza kwani wanaonyesha uwezo mzuri, naamini kwa kikosi tulichonacho tutafanya vizuri zaidi kwenye ligi,î alisema  Nsajigwa.

Siasa yaingia soka Iringa

$
0
0

Twalib Muwa, Iringa
UONGOZI wa chama cha soka wilaya ya Iringa mjini umemtangaza aliyekuwa katibu mkuu wa TFF, Fredirick Mwakalebela kuwa mdhamini mkuu wa ligi ya wilaya  itakayoanza mapema mwezi huu.

Akizungumza na Mwananchi katibu mkuu wa chama soka wilayani humo IMDFA, Bakari Kamtande amesema udhamini wa Mwakalebelela umepitishwa kufuatia makubaliano ya vipengele vilivyopo kwenye mkataba wao wa ligi hiyo.

Amesema Mwakalebela alikubaliana na vipengele vyote vya mkataba huo sambamba na kutaka kudhamini ligi hiyo kwa miaka mitatu kitu ambacho FA wilaya ilikataa na kumpatia miaka miwili pekee ya kudhamini ligi hiyo.

Kwa upande mwingine Kamtande amesema kuwa amesikitishwa na kauli za mbunge wa jimbo la Iringa mjini, Mchungaji Peter Msigwa juu ya kukilalamikia chama hicho kwa kutengua dhamira yake kudhamini ligi hiyo.

"Mch. Msigwa alitamka maneno ya kukidharirisha chama cha soka katika mkutano wa hadhara kuwa  IMDFA imeingiza siasa na mianya ya rushwa kwenye mchezo wa mpira wa miguu wilaya Iringa.

Kamtande alisema walitoa nafasi kwa Mbunge huyo kudhamini ligi ila alikataa kukubali baadhi ya vipengele vya mkataba ndipo walipotoa nafasi hiyo kwa  Mwakalebela.

"Tunaheshimu mchango wa mbunge Msigwa katika kuleta maendeleo ya soka la Iringa ila anaiondoa heshima yake kutokana na uwajibikaji mbovu wa waratibu wake.

Naye Mwakalebela alisema amekubali ombi la IMDFA, lakini bado hajatoa maamuzi juu kusaini mkataba na hajajua kama kuna mvutano kati ya chama na Mch Msigwa.

Morocco, Milovan waanza tambo

$
0
0
Jessca Nangawe na Burhani Yakub,Tanga
KOCHA wa Coastal Union ya Tanga, Hemed Morocco amesema lengo lake ni kutibua rekodi ya Simba kesho kwa kuhakikisha timu yake inaibuka na ushindi kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Simba inaongoza ligi ikiwa imeshinda mechi zote na kutoka sare mechi moja, ambapo kesho itakuwa wageni wa Coastal Union katika mwendelezo wa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Morocco alisema wamejindaa vema kukabiliana na Simba wenye rekodi nzuri msimu huu kwani wataingia uwanjani kwa lengo moja tu la kupata pointi tatu.

"Ndiyo kwanza naanza Ligi Kuu nikiwa na timu hii, Coastal ni timu nzuri na iko katika nafasi nzuri, ninaamini Simba inafungika, lakini mchezo utakuwa mgumu," alisema Morocco ambaye amepewa kikosi hicho cha Coastal hivi karibuni baada ya aliyekuwa kocha mkuu Juma Mgunda kujiuzulu.

Naye kocha wa Simba, Milovan Cirkovic alisema wachezaji wake wako vizuri na wapo Tanga kwa ajili ya kuendeleza ushindi na kuchukua pointi tatu kutoka kwa Coastal Union.

Alisema anafahamu kwamba Coastal Union ni timu nzuri hata  wachezaji wake wanalitambua hilo hivyo hawataidharau watambana ili kuendeleza ushindi katika ligi hiyo.

"Wachezaji wote wako fiti na tumekuja Tanga kwa ajili ya kuendeleza ushindi," alisema Cirkovic.

Timu ya Simba iliwasili jijini Tanga Jumatano jioni na kufikia katika hoteli ya Nyinda Classic, ambapo imekuwa ikifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Mkwakwani.

Hata hivyo Katibu Mkuu wa Coastal Union, Kassim El Siagi alisema Simba isitegemee kupata ushindi kwenye uwanja wa Mwakwani.

"Katika hili nadhani linafahamika na kila mtu kwamba Coastal Union siyo timu ya kuiogopa Simba au Yanga hasa kwenye uwanja wetu wa nyumbani hivyo tunawahakikishia mashabiki wetu kwamba  tutachukua pointi tatu Jumamosi," alisema El Siagi.

Taswa yaishangaa Yanga kuwashutumu waandishi

$
0
0
Vicky Kimaro, Mwanza
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (Taswa) umesema kuwa umesikitishwa na kitendo hicho cha viongozi wa Yanga kuwatuhumu baadhi ya waandishi mkoani hapa kuwa walipanga kuwahujumu.
 Katibu mkuu wa Taswa, Amir Muhando alisema kitendo cha viongozi na wanachama wa Yanga kinasababisha baadhi ya waandishi kushindwa kutekeleza majukumu yao.

Kabla ya mechi ya Yanga na Kagera Sugar iliyofanyika Jumatatu iliyopita kwenye uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, viongozi wa Yanga walianza kuwapigia simu waandishi wawili wa kike kutoka Dar es Salaam na kuwatolea vitisho kwa madai kuwa wamefika mkoani Kagera kwa ajili ya kuhujumu timu yao ili ifungwe na kudai kuwa waandishi hao wanatumiwa na kundi la Friends of Simba.

Hata hivyo; Waandishi hao walikanusha kuhusika na kitendo hicho na kwamba wapo kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao ya kazi kama walivyoagizwa na ofisi zao na hakuna kitu chochote kinachoendelea kati yao.

Mashabiki wa Yanga maarufu ëMakomandooí pamoja na viongozi wa klabu hiyo walichukizwa zaidi na kitendo cha mwandishi wa Bingwa, Onesmo Kapinga kuripoti habari ya wachezaji wa klabu hiyo kulala mzungu wa nne kwenye hotel ya Smart mjini Bukoba.
 
Muhundo alisema Taswa inasikitika na kitendo hicho cha Yanga na wanachama wao kwani walichofanya ni kinyume na utaratibu kwani walipaswa kuwasiliana na ofisi zao kama kuna dosari yoyote ikiwa ni pamoja na Taswa badala ya kuwatisha  na kuwafanya washindwe kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

ìSekreterieti ya Taswa ilifanya mawasiliano ya haraka na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Kapinga ambaye alikuwa mkoani Kagera na amethibitisha pasi na chembe ya shaka kwamba vitisho hivyo vimewanyima fursa ya kutekeleza majukumu yao ya kazi.

ìTukio hili limetuhuzunisha kwa sababu licha ya kuwajengea hofu baadhi ya waandishi wa habari kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kazi kikamilifu, lakini linaweza kujenga chuki zisizo na msingi kati ya klabu hiyo na Taswa.îalisema Muhando

Alisema wanachama na mashabiki wa klabu kubwa hapa nchini Simba na Yanga wakubali changamoto za viwanjani na wasitake kutafuta mahali pa kupeleka lawama zao pale wanapoona matokeo mabaya kwa klabu zao.

ìSi nia ya Taswa kutetea udhaifu kama upo kwa baadhi ya waandishi wa habari, lakini tunaona kwa malalamiko yanayotolewa na baadhi ya makomandoo hao kwa wanahabari si mazuri na hoja zao hazina mashiko ni kutapatapa.

ìTunauomba uongozi wa Yanga uwakemee mashabiki wake wachane na mambo yasiyo na msingi ambayo hayana manufaa kwa klabu hiyo.

Alisema Kamati ya Utendaji ya Taswa inatarajiwa kukutana mwishoni mwa wiki ijayo kujadili suala hili la vitisho kwa wanahabari na pia itajadili masuala mbalimbali ikiwemo kutaja mkoa utakakofanyika Mkutano Mkuu wa mwaka wa chama.
Viewing all 166 articles
Browse latest View live