![Rais wa zamani wa Shirikisho la Ngumi la Tanzania (BFT), Alhaji Shaban Mintanga]()
James Magai
HATIMAYE Rais wa zamani wa Shirikisho la Ngumi la Tanzania (BFT), Alhaji Shaban Mintanga aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya kusafirisha dawa za kulevya, ameachiwa huru baada ya kusota mahabusu kwa miaka minne.Katika kesi hiyo, Mintanga alikuwa akikabiliwa na tuhuma za kula njama na kusafirisha dawa za kulevya zenye uzito wa Kg. 4.8 kutoka Tanzania kwenda nchini Mauritius kwa kuwatumia wachezaji wa timu ya Taifa ya Ngumi za Ridhaa.
Hata hivyo, jana Mintanga aliachiwa huru na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, bila kujitetea baada ya mahakama kuridhika kuwa hana kesi ya kujibu.
Katika uamuzi wake wa kama mshtakiwa ana kesi ya kujibu au la, Jaji Dk Fauz Twaib alisema kwamba ameridhika kuwa mshtakiwa hana kesi ya kujibu kwa kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake.
Wakati wa majumuisho ya hoja, Wakili wa Serikali Mkuu (PSA) Fulgence Rweyongeza alidai kuwa upande wa mashtaka umethibitisha mashtaka dhidi ya mshatakiwa na kwamba mshtakiwa ana kesi ya kujibu.
PSA Rweyongeza hata hivyo alidai kuwa ushahidi wao katika kesi hiyo ni wa kimazingira na kwamba ushahidi wa kimazingira ni bora zaidi katika kesi hiyo.
Ushahidi huo wa mazingira ambao upande wa mashtaka uliuegemea ni namba za simu zilizodaiwa kukutwa kwenye tiketi za watu wanaodaiwa kukutwa na dawa hizo nchini Mauritius.
PSA Rweyongeza alidai kuwa shahidi wa kwanza, Christopher Mutabarukwa ambaye alikuwa Makamu wa Rais wa BFT alidai kuwa namba hizo za simu ni namba za mshtakiwa.
Ushahidi mwingine ni ushahidi wa shahidi wa pili wa upande wa mashtaka, Nassoro Michael Irenge aliyekuwa kocha wa timu hiyo wakati wanaenda nchini Mauritius.
Katika ushahidi wake, Irenge alidai kuwa watu waliokamatwa na dawa hizo walitambulishwa kwake na mshtakiwa kuwa wataambatana na timu hiyo kama mashabiki.
Hata hivyo katika uamuzi wake jana, Jaji Dk Twaib alisema kuwa katika kesi hiyo ushahidi wa moja kwa moja ulikuwa ni bora zaidi.
Alisema kuwa inawezakana kuwa mahakama ikamtia hatiani mshtakiwa kwa kutumia ushahidi wa mazingira mahali ambapo ushahidi huo wa mazingira haumgusi mtu mwingine zaidi ya mshtakiwa kuwa ndiye aliyetenda kosa husika.
Jaji Dk Twaib alisema kwamba anakubaliana na hoja za mawakili wa utetezi, Jerome Msemwa, Yassin Membar na Berious Nyasebwa kwamba kati ya mashahidi wote wanne wa Jamhuri, hakuna hata shahidi mmoja aliyetoa ushahidi unaomgusa mshtakiwa kiasi cha kumtaka apande kizimbani kujitetea.
Pia, Jaji Dk Twaib alikubaliana na hoja za utetezi kuhusu udhaifu wa shahidi wa upande wa mashtaka, husasani mkanganyiko wa maelezo ya mashahidi na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani mambo ambayo yanamnufaisha mshtakiwa huyo.
Miongoni mwa udhaifu huo wa ushahidi wa upande wa mashtaka ni pamoja na tofuti ya uzito wa dawa alizokuwa akihusishwa nazo mshtakiwa.
Hoja nyingine ya upande wa utetezi ambayo Jaji Dk Twaib alikubaliana nayo ni kuwa hakuna kielelezo cha dawa hizo kilichowasilishwa mahakamani hapo kama kielelezo, kama Wakili Msemwa alidai kuwa hakuna hata picha ya dawa hizo.
Akizungumzia hoja za mawakili wa utetezi kuwa kama hakuna shahidi hata mmoja aliyeweza kueleza jinsi ambavyo mshtakiwa alihusika katika dawa hizo kwa nini mshatakiwa alazimike kujitetea, Jaji Dk Twaib alisema,ì Sioni sababu ni kwa nini (mshtakiwa ajitetee).î
Jaji Dk Twaib pia alikubaliana na hoja za upande wa utetezi kuwa hakuna ushahidi kuthibitisha kuwa dawa hizo kweli zilikuwa ni dawa za kulevya kwa kuwa hakuna hati ya uthamini ya dawa hizo iliyoandaliwa na Kamishna wa Kudhibiti Dawa za Kulevya.
ìHuu ni udhaifu mwingine wa ushahidi wa upande wa mashtaka. Kamishna mwenyewe hakuweza kuziona dawa hizo (zilikuwa zikidaiwa kuwa ni za kulevya), na alishughulikia taarifa za mazungumzo kwenye simu tu,î alisema Jaji Twaib na kuongeza:
ìNina mashaka kama hii inatosha kuthibitisha kuwapo kwa dawa za kulevya na utendaji wa kosa la kusafirisha dawa za kulevya.î
Akizungumzia mkanganyiko wa uzito wa dawa hizo, Jaji Dk Twaib alisema kwamba kwenye hati ya mashtaka inadaiwa kuwa zilikuwa kilogramu 4.8 wakati kwenye fax (iliyotumwa kutoka Mauritius) inasema kuwa zilikuwa kilogramu 6.
Alisema hakuna shahidi yeyote aliyetoa ushahidi kuhusu asili na uzito wa dawa hizo.
Pia Jaji alizungumzia utata wa ushahidi wa shahidi wa nne mpelelezi wa kesi hiyo, Charles Ulaya ambaye alidai kuwa watuhumiwa wawili wanaoshikiliwa nchini Mauritius walimwambia kuwa walipewa dawa hizo na mtu waliyemtaja kwa jina la Mika na kwamba hawamjui Mintanga.
Pia Jaji alikubaliana na hoja za mawakili wa utetezi Msemwa na Nyasebwa kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kueleza mahali na muda ambao mshtakiwa alikula njama za kutenda kosa hilo.
ìKwa matokeo hayo, ninamuona mshtakiwa kuwa hana hatia. Chini ya kifungu cha 293 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, ninamuachia huru kwa mashtaka yote yaliyokuwa yakimkabili na anapaswa kuachiwa mara moja isipokuwa kama ataendelea kushikiliwa kisheria kwa makosa mengine,î alisema Jaji Dk Twaib.
Wakizungumzia uamuzi huo, mawakili wa Mintanga walielezea kufurahishwa kwao kwa kuwa wamepambana kwa muda mrefu kuhakikisha haki inatendeka na hatimaye imetendeka.
Msemwa alisema kuwa walikuwa wameiachia mahakama kwani ndio yenye uamuzi wa mwisho na kwamba wanafurahia sana huku Nyasebwa akisema kuwa wameuangusha mbuyu (Jamhuri ya Muungano wa Tanzania).
Matumaini ya Mintanga kuachiwa huru katika hatua hii ya awali ya kutokuwa na kesi ya kujibu yalianza kuchomoza Agosti 29, baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali maombi ya upande wa mashtaka kuongezewa muda wa kuwaita mashahidi wao waliodai kuwa ndio muhimu katika kesi hiyo.
Mashahidi hao ni watanzania watatu waliokuwa katika msafara wa timu hiyo kwenda Mauritius wanaokabiliwa na kesi kama hiyo ya dawa za kulevya walizokamatwa nazo nchini humo na maafisa wawili wa Serikali ya Mauritius.
Kutokana na mashahidi hao kukabiliwa na kesi hiyo nchini Mauritius, kesi ya Mintanga imekuwa ikiahirishwa mara kwa mara kutokana na maombi ya upande wa mashtaka ukiomba kuongezewa muda wa kuwaleta nchini kuja kutoa ushahidi dhidi ya Mintanga bila mafanikio.
Jambo hilo liliwalazimu mawakili wa Mintanga, Berious Nyasebwa kutoka kampuni ya Uwakili ya Member Law Attorneys na Aliko Mwamanenge wa Kampuni ya Msemwa & Co. Advocates kuiomba Mahakama itumie mamlaka yake kuilazimisha Jamhuri kufunga ushahidi wake.
Akitoa uamuzi jana Jaji Dk Twaib alitupilia mbali maombi hayo ya Jamhuri na kuamua kufunga ushahidi wa upande wa Jamhuri huku akiagiza pande zote kuwasilisha majumuisho ya hoja iwapo mshtakiwa ana kesi ya kujibu au la.
Katika uamuzi wake Jaji Dk. Twaib alisema kuwa katika kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa pande zote alitoa muda wa kutosha kwa Jamhuri kuwaleta mashahidi wake hao bila mafanikio na kwamba imeonesha kufanya uzembe katika suala hilo.
Alisema kuwa kila mara Jamhuri imekuwa ikiomba ahirisho kwa madai ya kuwaandaa mashahidi wake, jambo ambalo limekuwa likichelewesha mwenendo wa kesi hiyo na hivyo kupoteza muda wa mahakama.
ìHivyo mahakama inatumia mamlaka yake chini ya kifungu cha 264 cha CPA (Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai),îalisema Jaji Dk Twaib na kuamuru pande zote ziwasilishe majumuisho ya hoja kama mshtakiwa ana kesi ya kujibhu au la.
Mitanga alikuwa akidaiwa kushirikiana na watu wengine ambao hawajafikishwa mahakamani hapo, waliokuwa kwenye msafara wa timu hiyo iliposafiri kwenda kushiriki michezo ya ngumi nchini humo mwaka 2008, ambapo walitiwa mbaroni kwa tuhuma za kuingiza dawa za kulevya nchini humo.
Wanaodaiwa kukamatwa na dawa hizo nchini humo ni pamoja na kocha wa timu hiyo Nassoro Michael Irenge, Bondia Patrick Emilian, Petro Mutagwa na watu wengine wawili waliodaiwa kuwa ni mashabiki Charles Nathaniel na Rajabu Msengwa.
Hata hivyo; Irenge na Emilian walishaachiwa huru na kurejea nchini baada ya kubainika kuwa hawana hatia, lakini bondia Mutagwa na wengine waliodaiwa kuwa ni mashabiki pamoja na mwanamke mmoja raia wa Kenya bado wanashikiliwa mahabusu nchini humo.